2 Samuel 2

Daudi Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme Wa Yuda

1 aIkawa baada ya mambo haya, Daudi akamuuliza Bwana, “Je, nipande kwenda katika mojawapo ya miji ya Yuda?”

Bwana akasema, “Panda.”

Daudi akauliza, “Je, niende wapi?”

Bwana akajibu, “Nenda Hebroni.”

2 bBasi Daudi akakwea kwenda huko pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. 3 cPia Daudi akawachukua watu waliokuwa pamoja naye, kila mmoja na jamaa yake, nao wakaishi huko Hebroni na miji yake. 4 dNdipo watu wa Yuda wakaja Hebroni, huko wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.

Daudi alipoambiwa kuwa ni watu wa Yabeshi-Gileadi waliomzika Sauli,
5 eakatuma wajumbe kwa watu wa Yabeshi-Gileadi kuwaambia, “Bwana awabariki kwa kuonyesha wema huu kwa kumzika Sauli bwana wenu. 6 fSasa Bwana na awaonyeshe wema na uaminifu, nami pia nitawaonyesha wema ule ule kwa kuwa mmefanya jambo hili. 7 gSasa basi, kuweni hodari na mashujaa, kwa maana bwana wenu Sauli amekufa, nayo nyumba ya Yuda imenitia mafuta niwe mfalme juu yao.”

Vita Kati Ya Nyumba Ya Daudi Na Sauli

8 hWakati huo Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Sauli, alikuwa amemchukua Ish-Boshethi mwana wa Sauli na kumleta hadi Mahanaimu. 9 iAkamweka awe mfalme juu ya nchi ya Gileadi, Waasheri,
Waasheri hapa ni kabila moja la Israeli.
Yezreeli, Efraimu, Benyamini na Israeli yote.

10Ish-Boshethi
Ish-Boshethi maana yake Mtu wa Aibu, pia anaitwa Esh-Baali maana yake Mtu wa Baali ( 1Nya 8:33; 9:39 ).
mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala Israeli, naye akatawala miaka miwili. Hata hivyo, nyumba ya Yuda ikamfuata Daudi.
11 lMuda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ilikuwa miaka saba na miezi sita.

12 mAbneri mwana wa Neri, pamoja na watu wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. 13 nYoabu mwana wa Seruya na watu wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili.

14 oNdipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame na wapigane ana kwa ana mbele yetu.”

Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.”

15Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watu wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili. 16 pKisha kila mtu akakamatana na mpinzani wake kichwani na kuchomana kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu.
Helkath-Hasurimu maana yake Uwanja wa Mapambano.

17 rSiku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na watu wa Israeli wakashindwa na watu wa Daudi.

18 sWana watatu wa Seruya walikuwako huko: nao ni Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa. 19Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati akimfuata. 20Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?”

Akamjibu, “Ndiyo.”

21 tNdipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana wa kiume na umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza.

22 uAbneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?”

23 vLakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa.

24 wLakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni. 25Ndipo watu wa kabila la Benyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima.

26 xAbneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?”

27 yYoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao mpaka asubuhi.”

28 zBasi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Israeli tena, wala hawakuwapiga tena.

29 aaUsiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu.

30Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watu kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea. 31Lakini watu wa Daudi walikuwa wamewaua watu wa kabila la Benyamini 360 waliokuwa pamoja na Abneri. 32 abWakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na watu wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.
Copyright information for SwhKC